Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay na Dieng wawataka viongozi wa Sudan Kusini waache ubinafsi

Pillay na Dieng wawataka viongozi wa Sudan Kusini waache ubinafsi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, jana, amezungumza kwa simu na raisi wa Sudan Kusini Salva Kiir ili achukue hatua ya kusitisha uhalifu unaoendelea na kusaka watekelezaji wa mauaji ya Bor na Bentiu : ni ujumbe huo huo uliopelekwa asubuhi hii mbele na Navi Pillay kutoka Ofisi ya Haki za binadamu akiwa ziarani nchini humo. Taarifa kamili na Alice Kariuki

Akizungumza na waandishi wa habari, Navi Pillay amesema kwamba alikutana na viongozi wa pande zote za mzozo ambao umekuwa ukiendelea kwa miezi mitano, na kukiri kusikitishwa na kuona jinsi hali ya amani na matumaini ya nchi mpya ya Sudan Kusini vimezorota kwa kipindi cha muda mfupi.

Ameongeza kwamba hali inavyozidi kuwa tete, na kuongezeka kwa mauaji ya kujilipiza kisasi na kauli za chuki hasa baina makabila ya Dinka na Nuer, kuna hatari ya kuwepo kwa janga kubwa kwa raia wa Sudan. Ameshangaa kuwa viongozi wanaonyesha kutojali hali ya raia wao zaidi ya milioni 4 wanaoelekea kuteseka njaa kwa miezi ijayo.

Amesema, alipokutana na mkuu wa Upinzani Daktari Riek Machar, alimwambia hivi :

“ Nimetembelea kijiji hiki ili kukutana nawe, na nimeona watoto wakiwa uchi kwenye matope. Kweli maisha ya baadaye ya watoto hawa ni yapi ? Inabidii uwe na nuru kwa nchi hii. Nawaomba viongozi hawa wawili, kutojali mambo yao tu ya kibinafsi, lakini kujali pia hatma ya Sudan Kusini”

Halikadhalika amewapongeza viongonzi hawa kuonyesha nia ya kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi juu ya mauaji ya kikabila yaliyotokea Bentiu na Bor.

Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng ambaye naye pia alikuwa ziarani Sudan Kusini, amesema kwamba ni lazima kuchukua hatua haraka ili Sudan Kusini isielekee katika mauaji ya kimbari.

“ Hatupaswi kuacha Sudan Kusini kuelekea katika hii njia ya mashaka. Nawaomba wote kuchukua hatua za moja kwa moja kusitisha ghasia, na kuwajibika ili kulinda raia wa Sudan dhidi ya mauaji ya kimbari, ya kikabila, na uhalifu wa kivita na dhidi ya kibinadamu. Dunia inawatazama, na waliotekeleza uhalifu huo watawajibishwa.”