Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya WHO kuhusu usugu wa kiua vijisumu duniani ni tishio kwa afya ya umma:WHO

Ripoti ya WHO kuhusu usugu wa kiua vijisumu duniani ni tishio kwa afya ya umma:WHO

Shirika la afya duniani WHO limetoa ripoti ya kwanza ya aina yake kuhusu usugu wa dawa ikiwemo kiua vijisumu au antibiotics duniani kote. Tafiti hiyo ambayo ni ya kwanza imeonyesha kwamba changamoto hii kubwa sio mwelekeo wa siku zijazo bali ni jambo ambalo linashuhudiwa katika maeneo yote ulimwenguni na kuna uwezekano wa kuathiri mtu yeyote, wa umri wowote katika nchi yeyote.

Kulingana na ripoti hiyo, usugu wa kiua vijisumu unatokea wakati bacteria zinapobadilika na hivyo maambukizi hayawezi kutibiwa jambo ambalo linahatarisha afya ya umma.

Dr Keiji Fukuda msaidizi mkurugenzi mkuu kwa ajili ya usalama wa afya WHO amesema kwamba iwapo hatua ya pamoja ya wadau haitachukuliwa, dunia itajikuta katika zama za kutokuwepo na kiua vijisumu au antibiotics ambapo maambukizi ya kawaida na majeraha madogo madogo ambayo yamekuwa yakitibiwa kwa miongo mingi yatasababisha maafa.

Halikadhalika amesema kwamba kiua vijisumu ni sababu kubwa ambayo iliwawezesha binadamu kuishi kwa muda mrefu kwa afya bora na kunufaika kutokana na dawa za kisasa.