Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yalaani shambulio kwenye kituo cha afya CAR

UNICEF yalaani shambulio kwenye kituo cha afya CAR

Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF, limelaani shambulio lililotekelezwa dhidi ya kituo cha afya katika mji wa Boguila kaskazini mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mnamo Jumamosi Aprili 26, ambalo liliwaua raia 22 na wahudumu wa afya watatu kutoka shirika la matibabu ya kibinadamu la Médecins Sans Frontières (MSF).

Mkurugenzi wa UNICEF kwa ukanda wa magharibi na kati mwa Afrika, Manuel Fontaine, amesema mashambulizi dhidi ya vituo na wahudumu wa afya ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya watoto ya afya, na yanatatiza uwezo wa kutoa huduma ya dharura kwa wale wanaihitaji zaidi.

UNICEF imetoa wito kwa wale wanaozozana nchini CAR kuheshimu vituo vya afya kama taasisi za kibinadamu zisizoegemea upande wowote katika mzozo, na kama mahala salama pa kuwatibu watoto na watu waliojeruhiwa na wagonjwa.