Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akabidhi stakabadhi za Umoja wa Mataifa kwa CAR

Ban akabidhi stakabadhi za Umoja wa Mataifa kwa CAR

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, leo amekabidhi stakabadhi za Umoja wa Mataifa kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Toussaint Kongo-Doudou, katika hafla fupi iliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Stakabadhi hizo, zikiwemo Katiba ya Umoja wa Mataifa na kanda za DVD zenye kumbukumbu za tangu mwaka 1960, CAR ilipojiunga kwenye Umoja wa Mataifa kama mwanachama. Stakabadhi za Umoja wa Mataifa nchini CAR, ama zilipotea au kuporwa wakati wa machafuko ya hivi karibuni nchini humo, na ndiyo maana hizi mpya zikatolewa na Maktaba ya Dag Hammarskjöld, chini ya Idara ya Mawasiliano katika Umoja wa Mataifa, DPI.

Wakati wa hafla hiyo, Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa unafanya kila juhudi kuwasaidia watu wa CAR, kupitia utoaji wa huduma za kibinadamu, maafisa wa haki za binadamu kwenda huko kufanya uangalizi, na hata Baraza la Usalama kuidhinisha kuundwa kwa operesheni za kulinda amani, chini ya ujumbe mpya wa MINUSCA.

“Nilienda Bangui na nikajionea jinsi watu wanavyotaka amani. Umoja wa Mataifa u tayari kutoa misaada na huduma za kitaalam kadri uwezavyo kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mbali na hayo, kanuni zilizomo kwenye stakabadhi hizi zinaweza kusaidia kurejesha amani nchini mwenu na kuchangia ulimwengu wetu”