Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumizi ya silaha za kemikali hayahalalishwi kwa misingi yoyote ile: Ban

Matumizi ya silaha za kemikali hayahalalishwi kwa misingi yoyote ile: Ban

Ikiwa leo Aprili 29 ni siku ya kimataifa ya kumbukizi ya watu walioathiriwa na silaha za kemikali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amerejelea kile kilichotokea Syria mwaka jana wa 2013 akisema kuwa ni uhalifu wa kuchukuza zaidi dhidi ya binadamu na unatia doa kumbukizi ya mwaka huu.

Ban amesema picha za kutisha za wahanga wa shambulio hilo la silaha za kemikali kamwe hawezi kuzisahau akielezea kuwa ulikuwa ni ukatili mkubwa dhidi ya binadamu.

Ametumia fursa hiyo kusisitiza kuwa matumizi ya silaha hizo hayana utetezi wowote ule kwa misingi yoyote ile kwani ni ukiukaji wa itifaki ya mwaka 1925 na kanuni nyinginezo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Halikadhalika amezungumzia uteketezaji wa mpango wa silaha za kemikali Syria akisema kuwa ni ishara dhahiri ya kile kinachoweza kufanyika pindi jamii ya kimataifa inaposhikamana. Hata hivyo amesema hatua zaidi zahitajika kwani hadi sasa ni asilimia 92.5 tu za kemikali zote ndio zimeondolewa Syria.

Amesema Jamii ya kimataifa itatulia pindi silaha zote zitakapoondolewa na akataka siku ya leo itumike kurejelea ahadi ya kutokomeza silaha zote za kemikali.

Bwana Ban amesisitiza umuhimu wa mkataba wa kimataifa wa kupinga silaha za kemikali wa mwaka 1997 akizisihi nchi Sita ambazo hazijatia saini kufanya hivyo. Nchi hizo ni Angola, Misri, Israel, Jamhuri ya Kidemorasia ya watu wa Korea, Myanmar na Sudan Kusini.