Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini : msimu wa mvua waanza, UNHCR yakimbia kusaidia wakimbizi

Sudan Kusini : msimu wa mvua waanza, UNHCR yakimbia kusaidia wakimbizi

Wakati Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Navy Pilly anaendelea na ziara yake Sudan Kusini, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekiri wasiwasi wao kuhusu hali ya wakimbizi wa ndani nchini humo. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte

(Taarifa ya Priscilla)

Wakati mvua zinaanza maeneo ya Sudan Kusini, Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linajitahidi kutoa misaada ya awali kwa zaidi ya wakimbizi milioni moja waliopo Sudan Kusini.

Msemaji wa UNHCR, Fatoumata Lejeune, anaelezea wasiwasi;

“Nchini Sudan Kusini, UNHCR inahudumia raia ambao wana hofu sana, na hawana vifaa vya msingi, kwa sababu walilazimishwa kukimbia makwao kutokana na mzozo zaidi ya mara moja. Watateseka na mvua, kwa kuwa hawana jinsi ya kupika au kujisafi. Kwa jumla watu 923,000 ni wakimibizi wa ndani ambao wamesaka hifadhi katika maeneo 174 tofauti”

Msemaji huyo ameongeza kwamba zaidi ya watu milioni 4.9 wanahitaji msaada wa kibinadamu ambapo leo UNHCR imeanza msafara wa ndege kutoka Dubai ili kuwapatia raia 100,000 kutoka majimbo ya Unity, Jongley na Upper Nile vifaa kama ndoo, blanketi na magodoro.

Wakati huo huo , Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA, nchini Sudan Kusini Vincent Lelei, ametoa wito kwa pande zote za mzozo huo kusitisha mapigano yao kwa kipindi cha mwezi moja, ili kuwapatia raia mazingira yenye usalama wa kutosha ili waweze kupanda mazao kwenye mashamba yao.

Amesema msimu wa kilimo ni kati ya mwezi Aprili na Mei pekee na muda huo ukipitiwa raia watashindwa kuvuna kitu chochote hadi mwisho wa mwaka.