Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kitendo cha Maldives kutengua sitisho la adhabu ya kifo chatia wasiwasi

Kitendo cha Maldives kutengua sitisho la adhabu ya kifo chatia wasiwasi

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza masikitiko yake juu ya kanuni mpya iliyopitishwa nchini Maldives kutekeleza adhabu ya kifo, ikimaanisha kwamba sitisho la adhabu hiyo la miaka 60 linatupiliwa mbali.

Taarifa ya ofisi hiyo imesema kanuni hiyo mpya iliyoridhiwa na serikali tarehe 27 mwezi huu inatoa adhabu ya kifo kwa makosa ya nia ya kuua, ikiwemo hata kwa watu walio na umri wa chini ya miaka 18. Sheria nchini Maldives inatambua mtu kuwajibika na uhalifu akiwa na umri wa miaka 10 na hata kwa watoto wa umri wa miaka Saba.

Hii ina maana kwamba kanuni mpya inaweza kumtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo mtoto mwenye umri wa miaka Saba.

Hata hivyo watoto hao watasubiri hadi umri wa miaka 18 ndipo adhabu hiyo ya kifo itatekelezwa iwapo atapatikana na hatia ya kusudio la kuua. Vifungu ya namna hiyo kwenye kanuni mpya inaruhusu adhabu ya kifo kwa uhalifu uliotendwa na mtu pindi akiwa na umri wa chini ya miaka 18 jambo ambalo ofisi ya haki za binadamu imesema ni la kusikitisha na kutaka kanuni hiyo mpya itenguliwe..

Ofisi hiyo imeisihi serikali ya Maldives irejeshe sitisho la hukumu ya kifo katika mazingira yote hususan katika kesi zinazohusu watoto na kuchukua hatua kutokomeza kabisa adhabu hiyo.