Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uendelezaji teknolojia bunifu pekee haitoshi, bali zisambazwe: Ban

Uendelezaji teknolojia bunifu pekee haitoshi, bali zisambazwe: Ban

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa kutathmini mijadala ya kimataifa kuhusu uendelezaji na uenezaji wa teknolojia bora kwa maslahi ya dunia nzima. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi:

(Taarifa ya Assumpta)

Chimbuko la mjadala huo wa kwanza kati ya minne ni azimio namba 68/210 la mwezi Disemba mwaka jana lililopitishwa na baraza hilo wakati wa kuandaa ajenda endelevu baada ya mwaka 2015.

Akihutubia Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akasema ni wakati muafaka kwani ubunifu wa teknolojia zisizoharibu mazingira ni muhimu lakini muhimu zaidi ni kueneza ili ziweze kutumika na wote.

“Ushirikiano wa kiteknolojia ni harakati za muda mrefu. Chochote tutakachokubaliana kwenye mijadala hii minne kionekane kama mradi wa muda mrefu. Mawazo na ubunifu ni kama mali ya umma, na pindi mtu atakapoibuka na wazo la kipekee iwe kisayansi au kiteknolojia inatusaidia sote. Mathalani tunahitaji haraka teknolojia ya kupunguza kiwango cha gesi chafuzi. Kwa hiyo teknolojia nzuri ya mazingira inayozingatia mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi inaweza kuleta mchango wa kipekee kwenye jitihada hizi.”

Katibu Mkuu ametaka uendelezaji wa tafiti na maendeleo katika nchi zote na kwa kuanzia kuweka msingi stahili wa elimu hiyo kwa watoto wa kike na wa kiume.