Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM, IOM walaani shambulizi dhidi ya msafara wa watoa huduma za kibinadamu CAR

UM, IOM walaani shambulizi dhidi ya msafara wa watoa huduma za kibinadamu CAR

Huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR shambulio la Jumatatu dhidi ya msafara wa magari uliokuwa unahamishia eneo salama jamii ya waislamu limesababisha vifo vya watu wawili na wengine sita kujeruhiwa, jambo ambalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na lile la kimataifa la uhamiaji, IOM wamelaani.

Msafara huo wa magari 18 ukiwa na watu 1,300 ulikuwa ukitoka eneo la PK12 kuelekea Kabo na Moyen Sido kaskaizni mwa nchi hiyo na ulikumbwa na shambulizi la bomu linalosadikiwa kurushwa na wanamgambo wa Anti-Balaka.

Mwandishi wa Radio ya Umoja wa Mataifa aliyeko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jean-Pierre Ramazani anaelezea…

(Sauti ya Jean-Pierre Ramazani)

UNHCR pamoja na kulaani imetuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na kuelezea umuhimu wa kupatia ulinzi wakimbizi ambao maisha yao yako hatarini.

Hadi tarehe 22 mwezi huu CAR imekuwa na wakimbizi wa ndani zaidi ya 600,000 na miongoni mwao ni waislamu 15,000 ambao maisha yao bado yako hatarini kutokana na kwamba wamezingirwa na vikundi vya Anti-Balaka kwenye maeneo 15 magharibi mwa nchi hiyo.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kimataifa la uhamiaji IOM William Swing ameelezea kusitikishwa na shambulio hilo akisema kuwa madaktari na wauguzi wa shirika hilo wanaoambatana na msafara huo walitoa huduma za kwanza baada tu ya tukio.