Kampuni za kitaifa kutoka nchi zinazoendelea zazidi kupanua wigo wake nje ya nchi: UNCTAD

28 Aprili 2014

Ripoti ya robo mwaka ya Kamati ya Maendeleo na biashara duniani, UNCTAD imeonyesha ongezekola kampuni za kitaifa (TNC) kutoka nchi zinazoendelea kuwekeza katika mataifa mengine. Taarifa zaidi na Alice Kariuki.

(Taarifa ya Alice)

Ikiwa imezinduliwa leo, ripoti hiyo ya robo mwaka imeangazia mwelekeo na matarajio ya kampuni hizo katika uwekezaji ikimulika ni kampuni kutoka wapi na zinawekeza wapi. UNCTAD imesema uwekezaji kutoka kampuni za nchi zinazoendelea ulifikia kiwango cha juu mwaka 2013 na hivyo kufikia asilimia 39 ya uwekezaji wote duniani.

UNCTAD inasema miaka 15 iliyopita kiwango hicho kilikuwa asilimia 12 pekee na hivyo ni ongezeko kubwa ilhali kwa nchi zilizoendelea uwekezaji wa kampuni za kitaifa nje ya nchi umebakia kidogo, ikiwa pungufu kwa asilimia 55 ikilinganishwa na mwaka 2007.

James Zhan, Mkurugenzi wa kitengo cha uwekezaji na kampuni UNCTAD ametaja maeneo ya uwekezaji..

(Sauti ya Zhan)

Ni jambo la kuvutia kuona kuwa theluthi mbili ya uwekezaji huo ni katika nchi zinazoendelea,kwa hiyo wanawekeza katika nchi zinazoendelea na si zilizoendelea. Na habari haiishi hapo ni kwamba wanawekeza kwenye nchi nyingine zinazoendelea na nusu ya uwekezaji huo wanachukua mali za kigeni zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni za kitaifa za kigeni, TNCs.”

Afrika Kusini na Nigeria ni nchi zilizotajwa kuwekeza katika nchi zingine za Afrika ambapo kampuni za Afrika Kusini zinawekeza katika madini, maduka makubwa na mawasiliano ilhali Nigeria zinajikita kwenye huduma za fedha.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud