Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yatangaza kufungua uchunguzi wa awali nchini Ukraine

ICC yatangaza kufungua uchunguzi wa awali nchini Ukraine

Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC Fatou Bensouda amefungua uchunguzi wa awali wa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu nchini Ukraine.

ICC inasema kuwa ijapokuwa Ukraine si mwanachama wa mkataba wa Roma unaoanzisha mahakama hiyo, serikali mpya nchini humo iliridhia uchunguzi kufanyika kwa maelezo kuwa vitendo hivyo vilitekelezwa kati ya Novemba na Februari mwaka huu wakati wa maandamano ya kupinga serikali.

Uchunguzi utakaofanywa na ICC unapaswa kuhakikisha vigezo vya uchunguzi kwa mujibu wa mkataba wa Roma vinakidhi na ndipo uchunguzi kamili unaweza kuanza. Fadi El Abdallah ni msemaji wa ICC.

(Sauti ya Fadi)

“Mwendesha mashtaka atazingatia masuala kuhusiana na mamlaka ya ICC, ikiwemo aina ya uhalifu je ni uhalifu dhidi ya binadamu au mauaji ya kimbari ambayo yanaingia kwenye mamlaka ya ICC au la! Lakini pia masuala kuhusu maslahi ya haki na maslahi ya wahanga na uwezekano wa kuendesha kesi hizo hususan iwapo tuhuma husika ni makosa makubwa zaidi au hapana na iwapo kuna mashtaka au uchunguzi wa kina kwa ngazi ya kitaifa yanayofanana an tuhuma husika.”

Fadi amesema mwendesha mashtaka akiridhika kuwa vigezo vinakidhi kwa mujibu wa mkataba wa Roma ataomba kibali kwa mahakama na kufungua uchunguzi rasmi na iwapo la, basi atatangaza kumalizika kwa uchunguzi wa awali bila kuendelea na uchunguzi kamili.