Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa kingono kwenye maeneo ya migogoro ni sawa na bomu au risasi: Ban

Ukatili wa kingono kwenye maeneo ya migogoro ni sawa na bomu au risasi: Ban

Baraza la Usalama limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu wanawake, amani na usalama likiangazia ukatili wa kingono. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ukiukaji wa haki za binadamu kwenye migogoro ni janga kama lile liletwalo na bomu au risasi, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipohutubia mjadala huo akitanabaisha kuwa huleta machungu yasiyofikirika kwa wanawake, wanaume, wasichana na wavulana na hukwamisha maridhiano, amani na ujenzi mpya wa nchi.

Amesema baraza limepitisha maazimio kadha wa kadha kumaliza ukatili huo na kuna nuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Somalia ambako awali hata ubakaji haukuweza kujadiliwa.

Hata hivyo amesema juhudi zinaendelea ili kuongeza hatua za kutokomeza ukatili huo..

Jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utawala wa sheria na ukatili wa kingono kwenye mizozo linashirikiana na Colombia, Côte d'Ivoire, DRC, Guinea, Somalia na Sudan Kusini kuimarisha mifumo ya haki. Kila siku nchi nyingi zaidi zinajenga uwezo wa kiufundi kushughulikia ukatili wa kingono

Zainab Hawa Bangura ambaye ni mwakilishi wa Ban kuhusu ukatili wa kingono kwenye migogoro akatoa ombi rasmi la usaidizi kwa wahanga wa ubakaji akisema siyo tu wanawake na wasichana, bali familia na watoto waliozaliwa kutokana na ubakaji.

(Sauti ya Bangura)

"Hata kama hadi sasa wamenyimwa haki mahakamani, wahanga wanapaswa kufidiwa, usaidizi waweze kuishi, elimu kwa watoto wao na huduma za tiba na za kisaikolojia wanazopaswa kupatiwa na wanazohitaji.”

Mjadala huo wa wazi umeandaliwa na serikali ya Nigeria ambayo ndiyo inashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Aprili.