Kuwahamisha wakimbizi wa ndani CAR iwe hatua ya mwisho, wasema wataalam wa UM

25 Aprili 2014

Kuwahamisha wakimbizi wa ndani walio hatarini nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ili kuyalinda maisha yao kutokana na mashambulizi ya kidini inapaswa kuwa hatua ya mwisho kabisa, na ikiwa itachukuliwa, iwe tu baada ya mashauriano na wakimbizi hao, na kutimiza viwango wastani vya kimataifa. Hayo yamesemwa na wataalam wawili wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, Chaloka Beyani na Rita Izsak.

Chaloka Beyani, anayehusika na haki za wakimbizi wa ndani au IDPs, na Rita Izsak ambaye anahusika na haki za walio wachache katika jamii, wamesisitiza kuwa hata katika mazingira ambayo ni mabaya mno, ni vyema watu wanaohusika kuwezeshwa kufanya maamuzi yao wenyewe, na wasihamishwe kwa lazima.

Wamesema kwamba kufanya maamuzi magumu ya ama kukubali kuondolewa au kusalia waliko ni suala sugu sana kwa watu walio wachache kidini CAR, na hivyo basi ni vyema wakawezeshwa kufanya maamuzi hayo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud