Baraza la Usalama lalaani shambulio la kigaidi Algeria

25 Aprili 2014

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wamelaanu vikali shambulio la kigaidi dhidi ya raia wa Algeria, ambalo lilitekelezwa mnamo Aprili 19 kule Tizi Ouzou, na kusababisha vifo kadhaa na majeraha.

Katika taarifa iliyotolea na rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu, Balozi Joy Ogwu wa Nigeria, wanachama wa Baraza la Usalama wameelezea huzuni yao na kutuma risala za rambi rambi kwa watu na serikali ya Nigeria, na kwa wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo.

Wanachama hao wa Baraza la Usalama pia wamerejelea kusisitiza haja ya kukabiliana na hatari inayosababishwa na vitendo vya kigaidi kwa amani na usalama wa kimataifa, kwa kutumia mbinu zote chini ya Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa.

Wamesisitiza kuwa aina zote za ugaidi ni uhalifu ambao kamwe hazikubaliki, bila kujali umechochewa na nini, wapi unakofanyika, lini na nani anautekeleza, na usihusishwe na dini yoyote, utaifa au kabila lolote.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud