Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apongeza wananchi wa Algeria na serikali kwa mchakato tulivu wa uchaguzi

Ban apongeza wananchi wa Algeria na serikali kwa mchakato tulivu wa uchaguzi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amewapongeza wananchi pamoja na serikali ya Algeria kwa vile ambavyo uchaguzi wa Rais ulifanyika kwa amani.

Bwana Ban amesema hayo katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa ambapo ameeleza kuwa amefuatilia kwa karibu uchaguzi huo na kwamba alipeleka jopo la wataalamu watatu nchini humo kufuatia ombi la serikali. Jopo hilo lilifuatilia mchakato wa uchaguzi na kumpatia taarifa kila wakati wa kile kilichokuwa kinaendelea.

Amesihi serikali ya Algeria na vyama vyote vya siasa nchini humo kushirikiana kwa njia shirikishi na ya amani ili kuendelea utulivu na kuimarisha mchakato wa demokrasia nchini mwao.

Bwana Ban amerejelea msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuendelea kusaidia jitihada za Algeria za kufanya marebisho ya demokrasia pamoja na kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Algeria walipiga kura ya kumchagua Rais tarehe 17 mwezi huu ambapo Rais wa sasa Abdelaziz Bouteflika alichaguliwa kuendelea kuongoza nchi hiyo.