Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko lazima yakome hima Sudan Kusini

Machafuko lazima yakome hima Sudan Kusini

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa Hervé Ladsous ameonya kwamba hali ya machafuko inazidi nchini Sudani Kusini na kusisitiza kuwa licha ya juhudi za Umoja wa Mataifa kukomesha mapigano lakini jukumu la kuhakikisha machafuko yanakomeshwa linabaki mikononi mwa serikali ya Sudan Kusini.

Akiongea na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuhudhuria kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Bwana Ladsous amesema kinachoonekana sasa ni kukosekana kwa utashi wa pande kinzani kushiriki katika mazungumzo jambo linalokwamisha ukomeshaji wa machafuko.

(SAUTI LADSOUS)

Mfululizo wa machafuko ambayo yalianza tarehe 15 December mwaka jana lazima yakome, yakome hima. Tunaona kwamba hakuana upande ambao uko tayari kukomesha mapigano licha ya kusaini katika makubalainao miezi mitatu iliyopita. Pia tusisahau kwamba jukumu la msingi la ulinzi wa raia ni la serikali , tuko pale kusaidia lakini ni serikali ya Sudani Kusini kuhakikisha raia wake hawauwawi

Mkuu huyo wa operesheni za ulinzi katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa mapigano yamesababisha watu kukosa uhuru wa kutembea na hivyo kushindwa kuzalisha na kwamba baraza la usalama linafanyia kazi mambo hayo muhimu.