Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utawala wa Intaneti ni lazima ulenge kuwajumuisha wote: Ban

Utawala wa Intaneti ni lazima ulenge kuwajumuisha wote: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa utawala wa kutumia mtandao wa intaneti unapaswa kulenga kuwafikia watu wote na kuweka uwanja salama na unaowaunganisha watu kote duniani. Ban ameutoa ujumbe huo kwa mkutano wa mseto wa wadau kuhusu mustakhbali wa utawala wa intaneti, ambao unafanyika mjini Sao Paulo, Brazil.

Ban amesema intaneti inabadilisha maisha ya jamii tofauti katika kanda zote, na kwamba ni uti wa mgongo wa uchumi wa kimataifa, na muhimu kwa kusambaza habari na mawazo. Ameongeza kuwa ndiyo maana ni vyema kwamba sera za utawala wa intaneti ziendelee kuimarisha uhuru wa kujieleza pamoja na kusambaza habari kwa uhuru.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa intaneti ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo baada ya 2015, akitaja kuwa inaweza kuimarisha juhudi za kutokomeza umaskini, kuongeza usawa na kulinda rasilmali za sayari dunia. Amesema ili kuifikia ndoto hiyo, itabidi kupanua upatikanaji wa intaneti ili iwafikie takriban watu bilioni 4.3 ambao sasa hawana fursa ya kuitumia.

Hata hivyo, Ban amesema kuwa ni katika ujumuishaji wa watu wote tokea ngazi ya chini hadi juu ndipo itawezekana kuendeleza ndipo itawezeshwa intaneti inayowafikia wote, iliyo wazi na salama, na ambayo pia inaaminika.