Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tujali Mama Dunia kwa maendeleo endelevu na nishati mbadala: Ashe

Tujali Mama Dunia kwa maendeleo endelevu na nishati mbadala: Ashe

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, John William Ashe, ametoa wito kwa jamii ya Umoja wa Mataifa kuchagiza maendeleo endelevu na matumizi ya vianzo vya nishati mbadala katika miji na vijijini.

Hayo ni katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia, ambayo ni Aprili 22. Bwana Ashe ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na wadau wengine kuitikia wito uliotolewa mnamo mwaka 2009 katika azimio la Baraza Kuu wa kuwekeza zaidi katika teknolojia endelevu, na kuendeleza bayo anuai kupitia sera za kiraia  kimataifa kuhusu mazingira, hususan wakati huu inapochagizwa ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Rais wa Baraza Kuu amesema kuwa wakati tunapokabiliana na changamoto za aina yake za maendeleo endelevu, uelewa wetu wa mahitaji ya sasa na ya siku zijazo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira, ni lazima utokane na maelezo ya bora zaidi ya kisayansi, huku mikakati ya kimataifa ikichagiza maadili mema ya mazingira na kusisitiza uhusiano wa mwanadamu na mazingira.