Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini: Mauaji ya kikabila yatokezea Bentiu

Sudan Kusini: Mauaji ya kikabila yatokezea Bentiu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, umelaani vikali mauaji ya watu kwa misingi ya kikabila yaliyotokea Bentiu, Sudan Kusini. Taarifa na Joseph Msami:

UNMISS imethibitisha kuwa, baada ya wanajeshi wa SPLA walioasi kuuteka mji wa Bentiu, tarehe 16, April, waasi wao waliwaua mamia ya watu kutokana na uraia au kabila lao, wengine wakiwa wametafuta hifadhi hospitalini, hasa watu wenye kabila la Nuer, la Darfur, na makabila mengine.

Juu ya hiyo, UNMISS imelaani jinsi baadhi ya askari jeshi wa kundi hilo la SPLA walivyotumia radio Bentiu FM kusambaza ujumbe wa chuki ya kikabila na kutuma wanaume wa kabila moja kubaka wanawake wa kabila jingine.

Waasi wa SPLA – Mapinduzi walivamia Mskiti wa Kali-Ballee, ambapo walitenga watu kutokana na kabila lao, na kuwaua. Zaidi ya wananchi 200 waliuawa mskitini, na visa vingine viliripotiwa pia kanisani.

Hivi sasa, UNMISS imefanikiwa kuokoa watu zaidi ya 12,000 kutoka sehemu mbalimbali na kuwapa hifadhi ndani ya kambi la Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa UNMISS ameomba watekelezaji wa uhalifu huo wapelekwe mbele ya sheria, akitoa wito kwa pande zote za mzozo kuheshimu makubaliano yaliyotiwa saini mwezi wa kwanza mwaka huu.