Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lamulika uzuiaji wa mauaji ya kimbari

Baraza la Usalama lamulika uzuiaji wa mauaji ya kimbari

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limefanya kikao kuhusu uzuiaji na kukabiliana na mauaji ya kimbari, kama sehemu ya kukumbuka mauaji ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda miaka 20 iliyopita. Joshua Mmali na taarifa kamili

Baraza la Usalama limehutubiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, ambaye amesema mauaji ya kimbari nchini Rwanda, ni moja ya aya yenye uovu zaidi katika historia ya mwanadamu

Jan Eliasson

“Leo tunawakumbuka wahanga, tunawakumbuka manusura, tunapoendelea kufanya juhudi za kuwapatia haki, na kuzuia mauaji ya kimbari na mauaji ya halaiki popote duniani. Tunakumbuka kwa uzito mioyoni, kushindwa kwa jamii ya kimataifa kutambua na kuchukua hatua kufuatia onyo la mauaji ya kimbari. Ni lazima tuendelee kutumia msingi wa mafunzo tuliyojinfunza ili kuboresha uwezo wetu wa kuwalinda raia kutokana na uhalifu mbaya zaidi wa kimataifa”

Kikao cha leo cha Baraza la Usalama pia limehutubiwa na aliyekuwa rais wa Baraza la Usalama mwaka 1994, wakati mauaji ya kimbari yalipotokea, Colin Keating, ambaye ameomba msamaha

“Jukumu langu la kwanza hapa ni kuwakumbuka wahanga. Kikao hiki pia kinanipa fursa stahiki mimi binafsi kama rais Baraza la Usalama mwaka 1994, kuomba msamaha kwa kile tulichoshindwa kufanya mwaka 1994, na hilo liwekwe kwenye kumbukumbu rasmi za Baraza la Usalama”

Baraza hilo pia limepitisha kwa kauli moja azimio linalolaani kutokubali mauaji ya kimbari na kutoa wito kwa nchi wanachama kuahidi na kukabiliana na mauaji ya kimbari na uhalifu mwingine.