Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yathibitisha kifo cha Paul Sadala

MONUSCO yathibitisha kifo cha Paul Sadala

Charles Antoine Bambara, ambaye ni Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifia katika Jamhuru ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO, amesema kuwa MONUSCO imepokezwa Paul Sadala akiwa ameshakufa.

Paul Sadala akijulikana pia kwa jina la Morgan alikuwa ni kamanda wa kundi la Mai Mai Simba, ambaye alijisalimisha jumamosi iliyopita pamoja na wafuasi wake 42.

Msemaji wa MONUSCO ameileza redio ya OKAPI kwamba jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FADRC, waliiomba MONUSCO kuwasaidia katika zoezi la kumsafirisha kamanda huyo kutoka kijijini kwake mkoa wa Ituri, mashariki mwa DRC hadi Kinshasa. Aliongeza kwamba MONUSCO iliandaa utaratibu wa kumsafirisha kamanda yule, na ilipokutana na wanajeshi wa FADRC, mashambulizi yalikuwa yameshatokea katika FADRC na wafuasi wa Mai Mai ambapo Paul Sadala alipigwa risasi kwenye miguu miwili. Madaktari wa Monusco ambao walikuwa pale wakawahi kumhudumia lakini akafariki dunia wakati FADRC wakimpeleka ndani ya helikopta ya MONUSCO. 

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric naye alieleza kilichotokea ;

“ Dakatari wa Monusco walijaribu kumhuisha lakini wakashindwa. MONUSCO walishirikiana kwa kupokea maiti yake na hivi tunasubiri matokeo ya uchunguzi unaoendeshwa na Umoja wa Mataifa shambani kule. Uchunguzi wa Monusco unaoendelea sasa hivi utajaribu kutafuta wafuasi hawa 42 wa Mai Mai ambao hawajapatikana na kujua kilichotokea."