Baraza la usalama lalaani kutekwa kwa balozi wa Jordan huko Libya, lataka aachiwe huru

15 Aprili 2014

Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali shambulio dhidi ya msafara wa maafisa wa kibalozi wa Jordan nchini Libya, shambulio ambalo limefanyika leo na kusababisha kutekwa nyara kwa balozi wa Jordan nchini humo huku dereva wake akijeruhiwa.

Katika taarifa yao wajumbe hao wameeleza wasiwasi wao kuhusu shambulio hilo wakitaka balozi huyo aachiwe huru haraka iwezekanavyo huku wakisisitiza kuwa vitendo vya aina hiyo havihalalishwi kwa misingi yoyote ile.

Wametaka wahusika kufishwa mbele ya sheria wakikumbusha serikali ya Libya wajibu wake wa kulinda maafisa wa kibalozi na mali zao na kutaka izingatie wajibu wake wa kimataifa kwa mujibu wa mkataba wa Vienna na kuhakikisha anaachiwa kwa amani.

Baraza la usalama pia limerejelea azma ya jamii ya kimataifa ya kusaidia Libya katika kipindi hiki cha mpito cha kusaka amani na ustawi wa kidemokrasia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter