Baraza la usalama lafanya kikao cha dharura wakati ghasia Ukraine zikisababisha majeruhi:

14 Aprili 2014

Sinfotahamu inayoendelea kukumba Ukraine imelazimu Baraza la Usalama kukutana kwa dharura siku ya Jumapili ambapo Naibu Mkuu wa masuala ya siasa ndani ya Umoja wa Mataifa Oscar Fernandez-Taranco amesema kwa mara nyingine tena usalama nchini humo unazidi kuzorota.

Baraza hilo limekutana wakati huu ambapo saa 24 zilizopita zimeshuhudia mapigano kati ya wafuasi na wapinzania wa serikali ya Ukraine na Bwana Fernandez-Taranco ameonya kuwa mzozo huo unazidi kukomaa iwapo hatua thabiti hazitachukuliwa na pande zote kusitisha mzozo huo.

Fernandez-Taranco amesema wakati Baraza hilo linakutana kwa mara ya 10 kuhusu Ukraine, maeneo ya Luhansk, Kharkiv, Slavyansk na Donetsk na angalau miji mingine mitano mashariki mwa Ukraine yamekumbwa na mapigano hayo na kushikiliwa kwa majengo ya serikali.

Amenukuu waangalizi wa Umoja wa Mataifa kwenye miji hiyo wakisema kuwa watu wenye silaha wameweka vizuizi kwenye barabara na kwamba watu wapatao 50 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa Fernandez-Taranco mamlaka za Ukraine zimedhamiria kuwa iwapo vitendo hivyo visivyo halali vitaendelea, operesheni kamili ya kijeshi itaanzishwa.

Amemnukuu Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akisema kuwa hali sasa ni mbaya zaidi na kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unasisitiza suluhu kwa njia ya amani na pande zote kuheshimu sheria za kimataifa.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter