Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasi ya ongezeko la gesi chafuzi inatisha;IPCC yaonya, Ban ataka hatua zichukuliwe

Kasi ya ongezeko la gesi chafuzi inatisha;IPCC yaonya, Ban ataka hatua zichukuliwe

 Jopo  la kiserikali kuhusu mabadiliko ya tabia nchi limetoa tathmini yake ya tano inayendekeza jinsi ya kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi na kueleza kuwa kiwango cha utoaji wa gesi chafuzi duniani kinaongezeka kwa kasi kubwa na hivyo ni vyema hatua madhubuti zikachukuliwa.
Kufuatia kutolewa kwa ripoti hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekaririwa na msemaji wake akikaribisha ripoti hiyo inayopendekeza kupunguzwa kwa kiwango cha joto angalau kwa nyuzi joto Mbili kwa kipimo cha Selsiyasi.
Jopp hilo limesema hatua zikichukuliwa sasa gharama itakuwa ni ndogo kuliko kusubiri baadaye.
Mathalani IPCC imesema kuna njia ambazo bado ziko dhahiri za kupunguza utoaji wa gesi hizo za ukaa, njia ambazo jopo limesema zinatumia teknolojia  tofauti zinazowezesha dunia kutoa kiwango kidogo cha gesi na wakati huo huo uchumi endelevu kuimarika siku za usoni.
Kwa mantiki hiyo Bwana Ban ametaka mataifa kuchukua hatua haraka na kwa ujasiri ili yatangaze hatua madhubuti wakati wa mkutano wa viongozi kuhusu mabadiliko ya tabianchi mwezi Septemba mwaka huu na hatimaye kufikia makubaliano ya dunia mwakani.