Afrika inapeleka ajira zake nje badala ya kuzitengeneza kwa ajili ya watu wake

11 Aprili 2014

Wakati ripoti zinaonyesha kiwango cha ukuaji wa uchumi Afrika, Katibu Mtendaji wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya uchumi Afrika, UNECA Carlos Lopes amesema bado bara hilo halijaweza kutumia rasilimali na bidhaa zake kuweka fursa za ajira.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya uchumi barani Afrika kwa mwaka huu wa 2014 iliyojikita zaidi katika fursa za viwanda na ukwamuaji wa uchumi, Lopes amesema harakati za bara hilo kuendeleza viwanda zilikumbwa na mkwamo miaka ya Sabini kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo serikali kuingilia kati na mzozo wa mafuta wa mwaka 1972.

Bwana Lopes amesema bara la Afrika linazorotesha sekta yake ya uzalishaji kwa kuuza nje ya n nchi bidhaa badala ya kuziongezea thamani kabla ya kufanya hivyo.

"Afrika ina bidhaa nyingi na hivyo tuna uwezo wa kujadiliana vyema kuhusu bei ya bidhaa hizo. Tunafahamu kuwa mfumo mbaya wa bei unanyima Afrika karibu dola Bilioni 50 kwa mwaka na hilo ni jambo moja tu. Na rasilimali zote hizo kimsingi zinamaaanisha kwamba Afrika inapeleka nje ajira zake badala ya kuziunda. Kwa sababu uongezaji thamani wa bidhaa unafanyika nchi nyingineko ambako tunapeleka bidhaa zetu.”

Bwana Lopes amesema Afrika inahitaji kuwa na mfumo wa aina yake wa kuendeleza viwanda kwa kuzingatia mazingira na uhalisia wake na siyo kunakili yale ambayo yametekelezwa katika nchi zingine.