Mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu wa kivita na huenda ikawa uhalifu wa kibinadamu

11 Aprili 2014

Uhasama na mashambulizi ya kiholela dhidi ya wananchi Syria imekuwa jambo la kawaida amesema Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Bi. Valeri Amos.

Bi Amos amesema hayo baada ya shambulizi ambapo magari mawili yenye mabomu ya kutegwa yalilipuka katikati mwa mji wa Homs nchini Syria Jumanne na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20 na majeruhi zaidi ya 100 wakiwamo watoto na wanawake.

Ripoti zinasema kuwa watoa huduma wa kujitolea kutoka Shirka la hilali nyekundu Syria walijeruhiwa wakati bomu la pili lilipolipuka walipokuwa wakiwasili na gari la huduma za dharura kuwahudumia majeruhi wa bomu la kwanza. Jens Laerke ni Msemaji wa OCHA

Anasema kwamba ukatili na mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia yamekuwa yakifanyika kwa zaidi ya miaka mitatu Syria, na limekuwa jambo la kawaida. Lakini mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu wa kivita na yanaweza kuwa uhalifu wa kibinadamu. Matumizi ya mabomu ya kutegwa kwenye gari au kuangusha mabomu ya kutoka angani katika makazi bila kutofautisha walengwa kuwa jeshi au raia ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Halikadahalika Bi Amos amesema kwamba kugeuza watu kuwa vifaa vya vita, kuwatumikisha watoto jeshini na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni mambo ambayo hayakubaliki na yanapaswa kusitishwa. Ameongeza kwamba vita vina sheria na kwamba pande zote kwenye mzozo zinapaswa kuzingatia sheria ya haki za kibinadamu ya kimataifa.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter