Ripoti ya mwaka 2014 ya uchumi barani Afrika yazinduliwa leo

11 Aprili 2014

Hapa New York, leo kumefanyika uzinduzi wa ripoti ya mwaka 2014 ya uchumi barani Afrika. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Uchumi Afrika, sera bora za viwanda, michakato na taasisi bunifu ndiyo jina iliyopatiwa ripoti hiyo inayotolewa kwa pamoja kila mwaka na Umoja wa Maitaifa na Muungano wa Afrika, wakati huu ikielezwa kuwa bara hilo liko kwenye mwelekeo bora wa kujikwamua kiuchumi. Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya Afrika Maged Abdelaziz akasema viwanda vimepatiwa kipaumbele kwani katika mijadala na tafiti nyingi vimeonekana kuwa muhimu kwa maendeleo endelevu na kwamba...

(Sauti ya Maged)

Inajitikita katika maendeleo ya viwanda kama njia ya kufikia maendeleo endelevu na shirikishi, na maendeleo kwa kuzingatia vigezo vyote vinavyohusika navyo. Inashughulikia pia masuala muhimu ya jinsi taasisi za kijamii na kiuchumi za kikanda, Muungano wa Afrika pamoja na Umoja wa Mataifa zinaweza kufanya kazi kufikia malengo yake na inatoa mapendekezo kwa muktadha huo.”

Hata hivyo amesema sera shirikishi kuhusu viwanda ni muhimu ili maendeleo yaweza kutafsiriwa kwa kuwa na ajira zenye hadhi na ni matumaini yake kuwa Umoja wa Mataifa na wadau watasaidia Afrika kufikia malengo yake ya ukuaji wa uchumi kupitia uimarishaji wa sekta ya viwanda.