Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji miji iliyopangwa vyema, na uwezo wa kuongeza usawa: WUF7

Tunahitaji miji iliyopangwa vyema, na uwezo wa kuongeza usawa: WUF7

Kongamano la 7 la Kimataifa kuhusu Makazi ya Mijini, WUF7, linahitimishwa leo Ijumaa mjini Medellin, Colombia. Kongamano hilo liliwaleta pamoja takriban washiriki elfu kumi na tano kutoka nchi 164, ambao wamekuwa wakijadili kwa wiki nzima kuhusu aina za miji inayohitajika. Kutoka Medellin, Joshua Mmali anaripoti

RIPOTI YA JOSHUA

Mji wa Medellin, umetoa mfano kwa washiriki kwenye kongamano hili kuhusu jinsi ya kuendeleza miji na hivyo, ubora wa maisha ya wakazi wa mijini. Kauli mbiu ya jukwaa hili la mazungumzo imekuwa ni, ‘miji tunayoihitaji’. Nimemuuliza Dkt. Joan Clos, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat, ni aina zipi hizo za miji.

“Tunahitaji miji iliyopnagwa vyema, yenye maeneo zaidi ya umma, na uwezo wa kuitokomeza mianya inayoondoa usawa, ambayo sasa inaendelea kupanuka katika katika maeneo ya mijini. Si rahisi kufikia lengo hilo, lakini inawezekana. Inahitaji utashi wa kisiasa na uwezo wa kitaaluma. Labda lililo muhimu zaidi ni la kwanza: utashi wa kisiasa. Lakini pia unahitaji uwezo wa kitaaluma, kwani kuna vitu fulani ambavyo ni vya kitaalam na vinatakiwa kujulikana pia.”

Dkt. Clos amesema mipango ya miji inatakiwa kufanyika kwa njia ya kidemokrasi, kwa kuishirikisha jamii. Kwa kufanya hivyo, amesema watu watafuatilia harakati nzima, na hivyo kuwezesha mipango hiyo kufanikiwa. Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto uendelezaji wa miji unazokabiliana nazo, ambazo zimekuwepo tangu vita vikuu vya pili vya dunia, na kuwa sugu hata zaidi baada ya mdororo wa uchumi wa mwaka 2008

“Mtindo wa sasa wa ukuaji wa miji unaibua kutokuwepo usawa na ubaguzi wa maeneo na watu. Hili linaweka mipaka baina ya watu mbali mbali, na mipaka hii inaibua machafuko, manung’uniko. Nadhani tunatakiwa kuondoa dhana ya kwamba tunaweza kuwa na mji bora unaokidhi mahitaji ya kila mtu kwa njia ya usawa. Tunatakiwa kuwa na uelewa wa sehemu tofauti za jamii na kuwa na mazungumzo ya pamoja.”

Masuala muhimu katika kongamano hili yamekuwa ni usawa katika ukuaji wa miji na ushirikishaji wa wote ili kuwa na miji endelevu.