Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya kibinafsi inaweza kuchangia usawa mijini, wasema washiriki kwenye jukwa la Medellin

Sekta ya kibinafsi inaweza kuchangia usawa mijini, wasema washiriki kwenye jukwa la Medellin

Kikao cha saba cha Kongamano la Kimataifa kuhusu makazi ya mijini, kimeingia siku yake ya nne leo Alhamis, huku washiriki wakijadili mchango wa kampuni na biashara zinazomilikiwa na watu binafsi katika kufikia miji yenye usawa na endelevu kupitia utoaji wa huduma za kimsingi za mijini..

Wakati wa mijadala ya leo, washiriki wameelezea kutambua changamoto za ujenzi wa miji ambazo zimekuwepo kwa miaka mingi, huku wakitambua pia kuwa kuna changamoto mpya, ambazo hazijawahi kushuhudiwa zamani, na ambazo zinaibuka kila siku.

Wamesema changamoto hizi mpya zitahitaji ujuzi mpya, ufadhili na ufahamu wa mahitaji muhimu, hususan kwa watu maskini wanaoishi mijini. Patrick Magebhula kutoka Slum Dwellers International, Afrika Kusini, alikuwa mmoja wa wanajopo katika mjadala wa leo, ambao uliangazia biashara za watu binafsi na utoaji wa huduma muhimu.

“Uwezo ni fedha na ufahamu, ambavyo vinatokana na akiba ya kijamii, ushirikishwaji kikamilifu wa wanawake na mbinu nyingi na ubunifu wa jinsi ya kutoa kipaumbele kwa watu. Kutokana na kampeni ya ‘ujue mji wako’, mahitaji ya jamii yatajulikana: mahitaji ya kujisafi, maji na nishati, pamoja na aina zote za mahitaji ya watu maskini, kwa sababu ajenda huwekwa kutokana na mahitaji ya watu maskini”

Kongamano la 7 la Kimataifa kuhusu Makazi ya Mijini, linahitimishwa mnamo siku ya Ijumaa mjini Medellin, kwa azimio ambalo litatoa msingi wa mijadala ya mkutano wa tatu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat, ambao umepangwa kufanyika mnamo mwaka 2016.