Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lapitisha azimio la kuimarisha usalama barabarani

Baraza Kuu lapitisha azimio la kuimarisha usalama barabarani

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio lenye lengo la kuimarisha usalama barabarani wakati huu ambapo takwimu za shirika la msalaba mwekundu linasema kuwa watu 3,000 hufariki dunia kila siku duniani kutokana na ajali za barabarani.

Shirika la afya duniani WHO linasema asimilia 80 ya vifo hivyo ni katika nchi za vipato vya kati ambako ni nusu ya magari yaliyosajiliwa duniani  yanaendeshwa au kumilikiwa.

Akizungumza wakati anawasilisha azimio hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Urusi, Victor N. Kiryanov amelieleza kuwa ni la muhimu sana na kutaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kushughulikia tatizo la usalama barabarani kwa kupitisha mifumo sahihi ya udhibiti wa ajali na kuimarisha usalama barabarani.

Naye Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Samantha Power amesema utafiti unaonyesha kuwa watumiaji wa simu za mkononi wako hatarini mara tano zaidi kupata ajali  ya barabarani.

Amesema utumaji wa ujumbe mfupi wakati dereva anaendesha gari kunaweza kuchelewesha uchukuaji uamuzi sahihi sawa na dereva mwenye kiwango cha 0.08 cha pombe kwenye damu yake.

Balozi Power amesema nchini Marekani vijana wengi zaidi wanakufa kwenye ajali za barabarani si kwasababu wanaendesha magari wamelewa pombe bali kwa sababu ya kutuma ujumbe mfupi.