Hofu ya kinachoendelea Burundi: Ban azungumza na Marais wa Tanzania na Afrika Kusini

10 Aprili 2014

Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari, Adama Dieng yuko nchini Burundi ikiwa ni sehemu ya harakati za Umoja huo za kuepusha mzozo utokanao na udhibiti wa shughuli za kisiasa na ripoti zinazodai kuwepo kwa mpango wa kuwapatia mafunzo na silaha vijana wa chama cha CNDD-FDD

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric amesema ziara hiyo ya siku kadhaa ni sehemu ya jitihada za Umoja wa Mataifa za kuondoa wasiwasi wa kile kinachoweza kutokea nchini humo baada ya kupatikana kwa taarifa hizo.

Amesema tayari Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake huo kwa viongozi wa kikanda na kimataifa juu ya kile kinachoendelea kwa kuwa na mazungumzo na viongozi wa kikanda.

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu mkuu amejadili hali ya kisiasa nchini Burundi na Rais na makamu wa kwanza wa Rais wa nchi hiyo. Halikadhalika siku za karibuni amezungumza suala hilo na viongozi kwenye eneo hilo wakiwemo marais wa Afrika Kusini na Tanzania. Anatafuta usaidizi wao na kuisihi serikali ya Burundi kuchukua hatua mahsusi kushughulikia ripoti hizo.”

Bwana Dujarric akaenda mbali zaidi..

(Sauti ya Dujarric)

Tunasisitiza kwamba iwapo hakuna hatua inachukuliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unatokea, wale wanaohusika na kulaghai vijana wa vyama vya siasa kuchochea ghasia watawajibka kushtakiwa kimataifa.”

Msemaji huyo ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaamini Burundi itachukua hatua kwa kuzingatia kuwa inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwakani na kwamba ghasia za kisiasa zinaweza kuleta vurugu kubwa katika jamii.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter