Tutawafichua na kuwaumbua wanaofanya ukatili wa kingono: Bangura

9 Aprili 2014

Mwakilishi maalum wa Katibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya ukatili wa kingono Hawa Zainab Bangura amesema wanayopitia wanawake na watoto wanaokumbwa na ukatili wa kingono Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni machungu makubwa na kazi iliyobakia sasa ni kupeperesha bendera ya kuwatetea ili kuwafuta machozi yao.

Bi. Bangura amesema hayo katika mahojiano maalum na Stéphanie Coutrix wa Idhaa ya Kiingereza ya Radio ya Umoja wa Mataifa mjini New York baada ya uzinduzi wa ripoti kuhusu mafanikio na changamoto katika kutokomeza ukwepaji wa sheria wa ukatili wa kingono DRC.

Amesema kuna matumaini kupitia jitihada za Jamii ya kimataifa zinazoongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa za kuhakikisha sauti zao zinapazwa na kupigania vita vyao na kwamba….

(Sauti ya Bangura)

Tunafahamu wanakumbwa na unyanyapaa, lakini tunajitahidi kubadili mwelekeo kuhakikisha tunawafichua na kuwaumbua wanaume wanaofanya ukatili wa kingono na kuhakikisha tunawaadhibu. Kwa hiyo ujumbe kwa yeyote anayefanya ukatili wa kingono popote uliko na bila kujali wewe ni nani, tutakusaka na tutakupata.”