Ukatili wa kingono DRC, serikali ichukue hatua: Pillay asema!

9 Aprili 2014

Ofisi ya haki za binadamu ya umoja wa mataifa pamoja na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuweka utulivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO, zimezindua ripoti kuhusu mafanikio na changamoto katika kutokomeza ukwepaji wa sheria wa ukatili wa kingono nchini humo, ripoti hii ikitoa mapendekezo kwa wadau wote, hasa serikali ya DRC.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo mjini New York, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ameeleza takwimu zilizo ndani ya ripoti kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2010, hadi disemba 2013 zinazoonyesha kwamba wajumbe wa umoja wa mataifa wamesajili kesi zaidi ya 3600, nusu yake zikitokea Kivu Kaskazini, zikiwemo kesi za ukatili wa kingono kuanzia watoto wenye umri wa miaka 2 hadi za wazee wa miaka 80.

Amesema ubakaji unatumiwa kama silaha ya vita, kwa kutisha na kuwapa adhabu wananchi wakishukiwa kusaidia upande mwingine katika mgogoro ambapo vitendo hivyo vinatekelezwa mara kwa mara, wanawake wakienda sokoni, kuteka maji au wakiwa shambani kulima,

Navy Pillay amesisitiza kwamba wakati uhalifu huo unatekelezwa hasa na vikundi vya waasi, vikiwemo FDLR, ADL-NALU au Mai-Mai, lakini askari wa jeshi la serikali FADRC, wanatuhumiwa kushiriki pia kwa asilimia kubwa katika vitendo hivi.

Ingawa serikali ya DRC imejituma kupambana na ukatili wa kingono, nia hii nzuri haitoshi, na wala haijaonekana kwa ngazi za chini, Kamishna Mkuu amesema, akiongeza kwamba bado kuna hali ya ukwepaji wa sheria, ambao unasababishwa na ukosefu wa pesa na mafunzo katika mahakama na polisi zilizoko shambani, na pia aibu ya wahanga ambao wanaogopa kunyanyapaliwa na jamii zao.

Mwishowe, alisikitika kwamba wahanga hawa hawapati huduma mwafaka kama za afya, za kisaikolojikali na za kiuchumi.

Alitoa wito kwa serikali ya DRC :

“Naomba serikali ya DRC iiweke kipaumbele vita dhidi ya ukwepaji wa sheria wa ukatili wa kingono, naomba itekeleze uchunguzi unaofaa kwa haraka na njia huru, naomba ishtaki wanaoshukiwa, wakiwemo wanaojibika kwa ngazi za juu. Ni muhimu sana kuona mashtaka zaidi ya ukatili wa kingono”

Herve Ladsous, ambaye ni Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani ndani ya Umoja wa Mataifa ameeleza shughuli zinazoendelea chini ya usimamizi wa MONUSCO.

Amesema kwamba askari wa MONUSCO wamejituma sana kupambana na ukatili wa kingono, kwa kushirikiana na polisi ya DRC, akiongeza kwamba ni lazima serikali ya DRC ichukue hatua katika kuimarisha mfumo mzima wa sheria :

“ Kufungwa mhalifu gerezani hakuna maana wakati mhalifu huyo anaweza kukimbia kirahisi baada ya muda mfupi tu, na kuongeza kutendeka vitendo vilevile vya uhalifu. Kwa hiyo tunajutahidi sana kuhakikisha kuwepo kwa mfumo wa sheria wenye usawa na utashi. Inabidi tufanye kazi kuanzia vituo vya polisi vya kata, hadi mahakamani, na mfumo wa jela. Juu ya hiyo, tuwe wazi, inafaa kujenga upya mamlaka ya serikali hasa katika mikoa ya Kivu, ambayo inakumbwa na vita”

Bi Zainab Hawa Bangura, ambaye ni Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono, alishiriki pia katika utengenazaji wa ripoti hiyo na alipongeza bidii za serikali ya DRC katika vita dhidi ya ukatili wa kingono.

“ Mazungumzo ambayo nimeshiriki na raisi,ma seneta, viongozi wa jeshi na mahakama zinaonyesha kwamba viongozi wote wameongeza  hiari yao ya kisiasa kutokomeza ukatili huo unaoathiri wanawake, wanaume na watoto kwa muda mrefu mno. Kinachohitajika sasa ni kuendeleza utashi huo wa kisiasa na kuigeuza mabadiliko kwa ngazi za chini ili kulinda wananchi dhidi ya uhalifu wa haki za binadamu.”