Mjadala wa kina kuhusu ubia baada ya mwaka 2015 waanza UM

9 Aprili 2014

Hapa New York, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Kiuchumi na Kijamii wamekuwa na mjadala wa kina wa pamoja kuhusu dhima ya ubia kwenye utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015. Alice Kariuki na taarifa kamili.

(Taarifa ya Alice)

Maudhui ya mjadala huo ni kuangalia jinsi ubia unaweza kuongeza utashi katika malengo ya maendeleo ya milenia na pia kujenga ajenda ya baada ya mwaka 2015.

Akifungua mkutano huo, raisi wa baraza kuu la umoja wa mataifa, John Ashe, amesema tangu uzinduzi wa malengo ya maendeleo ya milenia, mwaka 2000, Umoja wa Mataifa umepambana na changamoto nyingi kutokana na hali ya kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi. Amesema hali hiyo imeonyesha jinsi dunia ilivyounganika siku hizi na umuhimu wa kushirikiana katika kuendeleza maendeleo endelevu. Ametaja ubia ambao unafaa kukabiliana na changamoto hizo.

(sauti ya Ashe)

“Msisitizo mwingi umeelekezwa kwenye kujenga ubia mpya katika ngazi ya kimataifa. Bila shaka hilo ni muhimu lakini kuna mengi ya kuzungumzia ambayo yanaweza kuimarishwa kupitia ngazi ya kitaifa na kikanda ambako kuna mambo mengi ya kufanyika na hatua za kuchukuliwa ili kujenga uwezo mpya.”

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon katika hotuba yake akasema..

(Sauti ya Ban)

"Viongozi wa dunia na wadau wengine wako katika fursa nzuri wakati huu tunaunda ajenda ijayo ya dunia. Hii ni fursa ya kuweka dunia yetu katika mwelekeo ambao ni wa mabadiliko, wenye usawa na endelevu.”

Washiriki wa mjadala huu wa siku mbili ni wawakilishi wa serikali, mashirika yasiyo ya serikali, taasisi mbali mbali, viongozi wa sekta ya kibinafsi, wasayansi, na wadau wa aina mbali mbali.