Tupanue mawazo ya kuendeleza nchi zetu ili yahusu miji: Prof. Stiglitz

9 Aprili 2014

Mshindi wa tuzo ya Nobel kuhusu uchumi, Profesa Joseph Stiglitz, amesema kuwa wakati watunga sera wanapofikiria jinsi ya kuendeleza nchi zao, ni vyema vilevile kufikiria jinsi ya kuendeleza miji. Akitoa mifano ya nchi kama Singapore, ambako makazi katika taifa zima ni mijini, Profesa Stiglitz amesema serikali zinaweza kuchangia pakubwa katika kuendeleza miji.

Mshindi huyo wa tuzo ya Nobel amesema vipimo bora vya maendeleo ya miji siyo katika pato la taifa au mji mzima, ila ubora wa hali ya maisha ya watu.

Amesema vipimo muhimu vya viwango vya hali ya maisha ni muda wanaopoteza watu kusafiri mijini katika misongamano na uchafuzi wa mazingira. Ameongeza kuwa miji inayofanya kosa la kutotambua hasara itokanayo na misongamano ya watu na uchafu, hupata hasara kubwa hata zaidi kiuchumi

“Muda unaopotezwa katika msongamano wa magari ndio muda ambao ungalitumiwa katika uzalishaji, uchafu huwafanya wawekezaji wasivutiwe kuwekeza katika miji isiyo safi, na pia madhara yake kwa afya, huchangia hata zaidi katika kuzuia uzalishaji”

Amesema kinachotakiwa kuangaziwa ni miji inayochangia na kuendeleza maisha bora, huku ikitoa kipaumbele kwa watu na uhai wao.