Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO : mlipuko wa Ebola ni changamoto kubwa

WHO : mlipuko wa Ebola ni changamoto kubwa

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema leo kwamba mlipuko wa Ebola unaendelea nchini Guinea na Liberia ambapo hadi idadi ya vifo vilivyothibitishwa kutokana na ugonjwa huo ni 72 kati ya watu 108 waliofariki dunia.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, mjini Geneva, Daktari Keiji Fukuda, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya usalama wa afya, WHO, alisema kwamba mlipuko huo unawapa changamoto zaidi kuliko milipuko mingine yote kuwahi kutokea hivyo akasema..

Sauti ya Fukuda

“ Sasa hivi tumethibitisha visa nchini Guinea na Liberia. Kwanza ni mlipuko hatari zaidi kuliko yote kwa kuwa eneo la visa ni pana sana. Cha pili, kupambana na Ebola ni kupambana na ugonjwa ambao unaua sana, na kutokana na hali hii, milipuko ya Ebola inasababisha hofu na wasiwasi kubwa katika jamii, inayosambaza uvumi mwingi. Kwa hiyo ni lazima kuwasialiana vizuri na vilevile kuwa makini sana katika mawasiliano haya”.

WHO imesema imeshapeleka wafanyakazi 50 katika maeneo yaliyoathirika na ugonjwa, ikitegemea kupambana na ugonjwa huu kwa kipindi cha miezi miwili hadi minne hadi itakapojiridhisha kuwa umetokomezwa.

Dokta Fukuda amesisitiza ushirikiano mzuri na wataalam wa Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Gabon ambao wamejitolea kuchangia uzoefu wao na kusaidia madaktari kwenye nchi hizo.

Halikadhalika amesema ni muhimu kujua kwamba kudhibiti maambukizo ya Ebola kunawezekana, kwa kutumia nyenzo za kujikinga, kama mfano kutambua mapema wagonjwa, kuzingatia taratibu za usafi hospitalini, na kuelimisha jamii.