Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usawa na uzalishaji wahitajika katika maendeleo ya miji: Ban

Usawa na uzalishaji wahitajika katika maendeleo ya miji: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ametoa wito hatua zichukuliwe ili kuweka mfumo mpya wa ukuaji wa miji wa karne ya 21. Katika ujumbe wake wa video kwa washiriki kwenye kongamano la 7 la kimataifa kuhusu makazi ya miji, Ban amesema mfumo huo mpya utawezesha kufikia miji endelelevu zaidi, iliyo jumuishi, yenye uzalishaji zaidi na usawa. Ban amesema ajenda ya maendeleo ya miji isimwache mtu yeyote nyuma

“Dunia yetu inaendelea kuwa yenye makazi ya miji. Hali hii inatoa fursa kubwa za maendeleo endelevu, ukuaji wa jamii wenye usawa, ukuaji wa kiuchumi jumuishi na mfumo bora wa mazingira”

Hata hivyo, Bwana Ban amesema kuwa licha ya fursa hizi, kuna changamoto kubwa, moja wapo ikiwa ni mwanya unaozidi kupanuka kijamii mijini. Ametoa wito kwa washirika kwenye kongamano la Medellin kufanya maendeleo jumuishi na kuutokomeza umaskini masuala ya kipaumbele katika mkutano wao wiki hii.

“Kote duniani, miji imegawanyika kwa misingi ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi. Watu wananyimwa nafasi za maisha bora ambayo mazingira ya mijini yanaweza kutoa na ambayo ni lazima yatoe. Tunahitaji maendeleo jumuishi ili kutokomeza umaskini wa kupindukia”

Pamoja na kutoa fursa ya kujadili hali ya miji duniani sasa, kongamano la Saba kuhusu makazi ya mijini (WUF7) linachukuliwa kama sehemu muhimu ya maandalizi ya mkutano wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa, UN Habitat III wa mwaka 2016, ambao utakuwa miongoni mwa mikutano ya kwanza ya kimataifa baada ya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.