Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasema uchumi wa CAR sasa mashakani

WFP yasema uchumi wa CAR sasa mashakani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mashauriano ya faragha kuhusu hali ya usalama na haki za binadamu kwenye nchi kadhaa za Afrika na huko Mashariki ya Kati. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

Miongoni mwa nchi ambazo Baraza linajikita kuangazia ni Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo machungu kwa wananchi yanaendelea kila uchao huku vikundi vyenye silaha ikiwemo Anti-Balaka vikiendelea kutishia usalama wa raia. Katika kikao hicho Kamishna mkuu wa haki za binadamu anatoa ripoti kuhusu hali ya haki za binadamu wakati huu ambapo mashrika ya Umoja wa Mataifa yanasema kuwa uchumi unaporomoka huku hali ya usalama ikiwa haitabiriki. Wakati huo huo Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Magharibi Denise Brown amezungumza mjini Geneva na kusema kuwa jamhuri ya Afrika ya Kati haipaswi kusahaulika kutokana na kile kinachoweza kutokea eneo hilo kwa kuzingatia alichoshuhudia hivi karibuni.

(Sauti ya Denise)

Wakati wengi wetu tunajikita kushughulikia mahitaji ya wakimbizi, twahitaji kutambua kuwa watu wameathirika hata kama siyo tu moja kwa moja na mzozo, wameathirika pia na hali ya uchumi, na kuna uwezekano kundi hilo litaongezeka baadaye kwa sababu nani atabakia kwenye nchi hiyo kuendesha uchumi. Nafikiri hili ni swali muhimu ambalo linasahaulika.”

Denise amesema WFP inajitahidi kusaidia wakimbizi hata nje ya mji mkuu Bangui ikiwemo Bossangoa, ambapo cha kusikitisha ni kwamba eneo la soko mjini humo limeteketezwa kabisa. Amesema hali ya usalama si nzuri.