Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMA yalaani mauaji ya waandishi wa habari Afghanistan

UNAMA yalaani mauaji ya waandishi wa habari Afghanistan

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afganstan UNAMA unalaani vikali shambulio la kuchukiza dhidi ya waandishi wawili wa habari wa kimataifa lililosabaabisha kifo cha mmojawao huku mwingine akijeruhiwa.

Waandishi hao wawili kutoka shirika la habari la Associated Press ni ripota Kathy Gannon na mpiga picha Anja Niedringhaus na walipigwa risasi jimboni Khost mashariki mwa Afghanistan wakati wakiwa katika shughuli ya kuripoti maandalizi ya uchaguzi wa Rais na majimbo unaofanyika kesho Aprili Tano.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa UNAMA Ján Kubiš amenukuliwa akisema amechukizwa na kile alichokiita shambulio la kigaidi dhidi ya raia na kuongeza kuwa waandishi hao walikuwa wanakwenda kazini kuufahamisha ulimwengu namna raia wa Afghanstan wanatekeleza haki yao ya kuandaa mutakabali wa wao, watoto wao na taifa lao.

Bwana Kubiš amesema shambulio hilo limesababisha nchi kupoteza watu muhimu ambao walikuwa wanaheshimiwa na kufahamika vyema kwa taaluma zao, upendo na thamani yao kwa watu wa Afghanistan na kujitoa kwao kueleza habari kuhusu nchi hiyo

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNAMA umetoa rambirambai zao kwa familia na ndugu kwa kifo cha mwanahabari na kumtakia majeruhi uponyaji wa haraka.