Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii zinazohifadhi wakimbizi wa Syria huko Lebanon zimezidiwa uwezo: OCHA

Jamii zinazohifadhi wakimbizi wa Syria huko Lebanon zimezidiwa uwezo: OCHA

Mkuu wa Ofisi inayoratibu usaidizi wa kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa, OCHA, Valerie Amos amehitimisha ziara yake huko Lebanon na kutaka jamii ya kimataifa kusaidia wananchi wa Lebanon wanaokumbana na changamoto kila uchao wanapohaha kukirimu wakimbizi kutoka Syria.

Amesema usaidizi huo uende sanjari na usaidizi kwa wakimbizi wa Syria kwani miaka mitatu tangu kuanza kwa mapigano nchini mwao hali inazidi kuzorota kila uchao, watoto hawaendi shule, huduma za afya hazipatikani na ustawi wa kiuchumi, kisiasa na kijamii nchini Syria sasa u mashakani.

Akiwa Lebanon, Bi. Amos ametembelea familia za wakimbizi wa Syria kwenye jimbo la kaskazini kabisa mwa nchi hiyo Akkar ambako machungu ya maisha yanazidi kadri siku mpya inavyoingia.

Watoto walimweleza hawaendi shule kwani wazazi wao hawawezi kulipa karo na akasema kizazi kizima sasa kiko hatarini.

amekutana pia na viongozi wa serikali ya Lebanona akiwemo Rais Michel Sleiman, Waziri mkuu Tammam Salam na kujadili jinsi gani jamii ya kimataifa inaweza kuendelea kusaidia Lebanon.

Robo moja ya kwaka ikiwa imemalizika, kumepatikana asilimia 14 tu ya ombi la dola Bilioni 1.7 zinazohitajiwa na mashirika ya misaada ya kibinadamu ili kuimarisha usaidizi wao huko Lebanon.