James Bond aungana na UNMAS kuhamasisha kuhusu madhara ya mabomu ya kutegwa ardhini

4 Aprili 2014

Leo ni siku ya kimataifa ya uhamasishaji na kutoa msaada wa kutokomeza matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini ambapo maudhui yake yanaangazia umuhimu wa wanawake katika shughuli hizo. Grace Kaneiya na Taarifa kamili.

Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amesema ni muhimu wanawake washirikishwe zaidi katika kuelimisha jamii, kusaidia waathirika na kuondoa mabomu ardhini.

Amesema uteguaji wa mabomu hayo unasaidia jamii kurejesha watoto shuleni, kurejelea ukulima na ufugaji vijijini, na kuokoa maisha ya watu na mifugo kwani katika sehemu zenye mabomu hayo jamii huwa na hofu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uteguaji wa mabomu ya ardhini, UNMAS, limesema kwamba hadi leo, kuna mabomu Milioni 110 katika nchi 70 zikiwemo Sudan, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. Daniel Craig ambaye ni mchezaji wa filamu kama James Bond anazungumza kwenye filamu ya mwanamke Betty anayeondoa mabomu Sudan Kusini na hapa anazungumzia anasema..

“Hofu inatawanyika. Ni hofu ambayo inaathiri uchumi na pia jamii nzima. Ni hofu ya kuwepo kwa mabomu ya kutegwa ambayo huenda hata hayapo. Lakini watajuaje ? Bomu hili la bei ndogo sana linagharimu dola 2 tu kulitega ardhini, lakini linagharimu karibu dola elfu 2000 kuligundua na kulitegua. Bomu hilo ni muuaji bila aibu wala huruma, linaua bila kubagua, awe mwanamke, mtoto, jeshi au mnyama. Limelala huku, kama askari ambaye yuko tayari muda wowote, bila kuhitaji usingizi wala chakula, bila kulalamika, liko tayari kufanya kazi yake chafu kwa kipindi cha miaka 30 na zaidi”