Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wakimbizi wa Syria nchini Lebanon yavuka Milioni Moja

Idadi ya wakimbizi wa Syria nchini Lebanon yavuka Milioni Moja

Nchini Lebanon, kati ya watu 1000, watu 220 ni wakimbizi kutoka Syria, hizo ni takwimu zilizotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR wakati huu ambapo idadi ya wakimbizi hao imevuka Milioni Moja.

UNHCR inasema miaka mitatu tangu kuanza kwa mzozo huo Lebanon imekuwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ikihaha kukidhi mahitaji yao kadri wanavyoongezeka huku dalili za wao kupungua zikiwa ni ndoto. Joelle Eid ni msemaji wa UNHCR nchini Lebanon na anaeleza kuwa sasa kinachohitajika si msaada wa fedha tu bali pia kusaidiana na Lebanon kuhifadhi wakimbizi hao.

(Sauti ya Joelle)

"UNHCR inashirikiana na mashirika mengine Sita ya usaidizi pamoja na serikali kuwapatia wakimbizi mahitaji muhimu pamoja na wenyeji ambao kwa miaka mitatu hii ya janga wamekuwa wakarimu kuwahifadhi. na wale wanaowahifadhi mahitaji muhimu. Bado kuna changamoto nyingine pia, makazi,elimu kwani tuna zaidi ya watoto Laki Tatu hawako shuleni, afya, ni ngumu sana kwa mkimbizi kupata huduma bora. Hii leo siyo tu tunahitaji fedha kwa ajili ya serikali na mashirika kutoa misaada muhimu, bali pia kusaidiana na Lebanon katika kuwahifadhi wakimbizi hao.”