UNFPA yaungana mkono na wadau kukabiliana na ndoa za utotoni Tanzania

3 Aprili 2014

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA limetiliana saini na taasisi ya Graça Machel na ile ya utu kwa mtoto CDF makubaliano yakupinga ndoa za utotoni nchini Tanzania. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Makubaliano hayo yamefanyika wakati Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi 41 duniani zenye idadi kubwa ya watoto wa kike wanaoozwa katika umri mdogo ambapo kwa wastani wasichana wawili kati ya watano wameolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Kaimu Mwakilishi mkazi wa UNFPA Tanzania Mariam Khan amesema Kupitia makubaliano hayo mashirika hayo yatashirikiana kwenye shughuli kama vile utafiti kwenye mikoa husika juu ya sababu za ndoa za utotoni.

Halikadhalika Kuwawezesha wasichana na wanawake kutetea haki zao kwa njia zinazokubalika na jamii yao, kuwajulisha haki za kisheria na kikatiba na kujenga uwezo wa kuelewa na kufanya kazi ili kupinga ndoa za utotoni. Sawiche Wamunza ni afisa wa UNFPA Tanzania

(Sauti ya Sawiche)

UNFPA inasema ndoa za utotoni zinakwamisha kufikia malengo ya milenia ikiwemo kuondoa umaskini, usawa wa kijinsia na afya ya mama na mtoto na hivyo ni muhimu kuwekeza kwa wasichana.

Inasema elimu zaidi na ndoa baadaye ndio kauli mbiu ya sasa kwani msichana atakayeolewa baadaye atakuwa na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi wa wakati wa kubeba ujauzito pamoja na idadi ya watoto.