Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tupatie ubongo wetu lishe bora kama tunavyolisha miili yetu:

Tupatie ubongo wetu lishe bora kama tunavyolisha miili yetu:

Wakati ulimwengu leo unaadhimisha siku ya kimataifa ya kuhamasisha vitendo kuhusu ulemavu wa akili kwa kuwasha mwanga wa bluu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema kadri siku zinavyosonga, watoto na watu wazima wenye ulemavu wa akili wanazidi kutengwa na jamii zao na hata katika jamii ambako wanajumuishwa bado wanakosa huduma za msingi.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake wa siku hii ya kuchukua hatua dhidi ya tatizo hilo la kiafya ambalo hujitokeza miaka mitatu ya mwanzo ya uhai wa binadamu.

Katibu Mkuu amesema ujumbe wa mwaka huu ni kufurahia fikra bunifu za watu wenye ulemavu wa akili ambao amesema katika fursa adhimu za kukutana nao zilimhamasisha na walionyesha uwezo mkubwa.

(Sauti ya Ban)

“Uthabiti wao unatupatia motisha. Wana haki ya kupatiwa fursa zote ziwezekanazo kwa ajili ya elimu, ajira na kujumuishwa.”

Kwenye Umoja wa Mataifa kulifanyika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu ugonjwa huo ambapo mtaalamu kutoka Bangladesh alitanabaisha alichogundua kwenye tafiti zake.

(Sauti ya Mshiriki)

“Kwa bahati mbaya nimebaini duniani kote, watu wanakula chakula kujaza matumbo yao au ladha waitakayo au kukidhi mifumo yao ya maisha.kamwe hawagundui kuwa mlo wa kila siku haukidhi mahitaji ya lishe ya mwili mzima. Na bahati mbaya hapo ndipo ninapoona kuwa mlo wa ubongo unakosekana. Iwapo ukila lishe ya kurubisha ubongo utaona kumbukumbu inarejea ndani ya mwezi mmoja. Hii ina maana gani? Ina maana kwamba unarutubisha chembechembe za ubongo.”

Dalili za mtoto mwenye ulemavu wa akili ni pamoja na mtoto kushindwa kutangamana na wazazi, familia, jamii kushindwa kucheza na hata kuwa na uwezo mdogo wa kupambanua mambo.