Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakuu wa WFP na UNHCR wasikitishwa na walichoshuhudia Sudan Kusini

Wakuu wa WFP na UNHCR wasikitishwa na walichoshuhudia Sudan Kusini

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wameonya kuwa janga linaloendelea Sudan kusini linaweza kuhatarisha maisha ya mamilioni ya watu katika miezi michache ijayo iwapo hakuna hatua za dharura zitakazochukuliwa kumaliza mgogoro unaoendelea na kusaidia raia wanaohaha kujikwamua.

Viongozi hao ni Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Antonnio Guterres na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP Etharin Cousin ambao wamehitimisha ziara yao ya siku mbili iliyowapeleka jimbo la Unity na kuwakutanisha na waathirika wa mapigano yanayoendelea pamoja na viongozi akiwemo Rais Salva Kiir na wahisani.

Mathalani Bi. Cousin amesema wanawake aliozungumza nao eneo la Nyal wamemtuma salamu tatu kwa jamii ya kimataifa ambazo ni kwamba wanataka Amani, usaidizi kumaliza machungu yao na fursa kwa watoto wao kurejea shule.

Guterres kwa upande wake amesema watu wengi hawapati misaada na kwamba mapigano yanafanya watu wasindwe kushiriki shughuli za kilimo.

Amesema inasikitisha kuona wakimbizi wa zamani waliorejea na matumaini wakianza tena kukimbia kuokoa maisha yao.

Rais Kiir amehakikishia viongozi hao kuwa watasaidia vifaa vya usaidizi kufikia wahitaji wakati huu ambapo tangu kuanza kwa mapigano Disemba 15 zaidi ya watu 800,000 wamekimbia makazi yao wakisaka hifadhi ndani au nje ya nchi yao.

Kesho wakuu hao wa WFP na UNHCR wanaelelekea ETHIOPIA ambako nako kuna wakimbizi kutoka Sudan Kusini.