Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano mapya CAR yazidisha machungu kwa raia

Mapigano mapya CAR yazidisha machungu kwa raia

Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa kwake na hali mpya ya mapigano huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ukitaka hatua za haraka kuchukuliwa kutekeleza ombi la Katibu Mkuu la kuimarisha vikosi vya ulinzi wa amani. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Amkani si shwari tena kwenye mji mkuu Bangui, ndivyo ofisi ya haki za binadamu ilivyoripoti ikisema tangu Kamishna Mkuu Navi Pillay ahitimishe ziara yake tarehe 22 mwezi uliopita, mapigano kati ya kikundi cha Anti-Balaka na waislamu kwenye viunga vya mji huo yamesababisha vifo vya watu wapatao 60 wakiwemo watoto. Halikadhalika Anti-Balaka wanakabiliana na askari wa kikosi cha Afrika, MISCA na hata wale wa Ufaransa. Cécile Pouilly anarejelea wito wa Pillay.

(Sauti ya Poully)

“Kwa kuzingatia uzorotaji huu wa hali ya usalama, kwa mara nyingine tena tunaomba nchi kuunga mkono wito wa dharura wa Katibu Mkuu wa kupeleka maelfu ya walinda amani na polisi.”

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema mapigano hayo mapya yamesababisha watu wengine 16,000 mjini Bangui kukimbia makazi yao na kufanya idadi kufikia 637,000. UNHCR inasema hali inatisha zaidi vitongoji vya Boda, Carnot na Berberati vya mjini Bangui. Fatoumata Lejeune-Kaba, msemaji wa UNHCR.

(Sauti ya Fatoumata)

“UNHCR na wadau wake wanapanga kutuma wafanyakazi eneo hilo wiki hii ili kubaini mahitaji ya kibinadamu na kuhakikisha usaidizi unafikia walio hatarini zaidi Boda na Carnot. Na kwa sasa tunaangalia uwezekano wa kuwahamishia Kabo na Moyen Sido kaskazini mwa nchi.”