Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuepushe migogoro badala ya kutumia muda mwingi na usaidizi baada ya kuibuka: OCHA

Tuepushe migogoro badala ya kutumia muda mwingi na usaidizi baada ya kuibuka: OCHA

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA imezindua ripoti yake inayotaka wahisani na mashirika mbali mbali kujikita zaidi katika kuzuia majanga badala ya mfumo wa sasa wa kutoa usaidizi majanga yanapotokea.

Ripoti hiyo iitwayo Okoa maisha leo na Kesho imezinduliwa mjini New York ikitia shime zaidi mtazamo mpya wa kuchukua hatua kushughulikia uepushaji wa majanga hayo kwani imeonekana kwa sasa msisitizo zaidi ni usaidizi watu wakishakumbwa na madhila hayo.

Naibu Mkuu wa OCHA Kyung-Wha Kang akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo amesema uchukuaji hatua mapema kutapunguza hata kiwango cha usaidizi kinachoombwa pindi majanga yanapotokea.

Mathalani amesema kwa miaka Kumi iliyopita mahitaji ya kibinadamu yameongezeka kwa kasi kubwa na hitaji la fedha halikadhalika limeongezeka kaw asilimia 430.

Amehadharisha kuwa wahisani nao wanajikuta katika hali ngumu kwani mahitaji ni zaidi ya uwezo wao na hivyo mwelekeo wa sasa si endelevu.

Bi. Kyung-Wha amesema mapendekezo ya ripoti hiyo ni pamoja na kupatia suluhu chanzo cha migogoro ili kuepusha isitokee na siyo kujikita tu na viashiria.