Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ziarani Ulaya na Afrika: Kesho kushiriki mkutano wa kimataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari

Ban ziarani Ulaya na Afrika: Kesho kushiriki mkutano wa kimataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon anaelekea Brussels, Ubelgiji ambapo kesho atajumuika kwenye siku ya pili ya mkutano wa kimataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari.

Mkutano huo ni sehemu ya shughuli za Bwana Ban barani Ulaya ambapo Jumatano atashiriki kikao cha viongozi wa Umoja wa Ulaya na Muungano wa Afrika na ule utakaoangazia Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Bwana Ban atakuwa pia na mazungumzo na Rais wa baraza la Muungano wa Ulaya na wa Tume ya Muungano huo na majadiliano pia na viongozi waandamizi wa Ubelgiji wakiwemo Mfalme Philippe na Malkia Mathilde.

Kutoka Ubelgiji tarehe Nne ataelekea Jamhuri ya Czech na kutoa mhadhara kwenye chuo kikuu cha Charles kuhusu dhima za nchi hiyo na Umoja wa Mataifa katika amani, maendeleo na haki za binadamu kwenye ulimwengu wa sasa.

Katibu Mkuu baadaye ataelekea Kigali ambako tarehe Saba Aprili atashiriki kumbukumbu ya miaka 20 ya mauaji ya kimbari.