Tunaondoka Sierra Leone tukijivunia mengi: UNIPSIL

31 Machi 2014

Tunaondoka wakati muafaka wakati Sierra Leone inachukua hatamu ya kusongesha mbele maendeleo yake, ni kauli ya Jens Toyberg-Frandzen, Mwakilishi mtendaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa ofisi ya ujenzi wa amani ya Umoja huo nchini Sierra Leone, UNIPSIL aliyotoa wakati huu ambapo ofisi hiyo imefunga rasmi pazia la jukumu lake Jumatatu 31 Machi.

Toyberg-Frandzen amesema katika mahojiano maalum kuwa jambo analokumbuka zaidi ni uamuzi uliosababisha kufungwa kwa ofisi hizo.

(Sauti ya Toyberg-Frandzen)

“Na hiyo ilikuwa ni mafanikio ya kipekee ambayo nchi hiyo ilipata wakati wa uchaguzi mwaka 2012 ambapo niliguswa sana nilipotembelea vituo mbali mbali vya kupigia kura, nikashuhudia wanawake wakiwa wamebeba watoto wao mgongoni wamepanga foleni kwenye jua tayari kutekeleza haki yao ya kupiga kura. Matokeo ni kwamba tulikuwa na uchaguzi wenye amani na serikali iliyowekwa madarakani kwa amani na hiyo ilikuwa ishara kwa dunia kwamba hii ni mara ya tatu wamefanya uchaguzi kwa amani na hivyo kwamba ulinzi wa amani hauna tena nafasi.”

Bwana Toyberg-Frandzen akaenda mbali zaidi kueleza ni jambo gani nchi nyingine zinaweza kujifunza kutoka Sierra Leone.

(Sauti ya Toyberg-Frandzen )

Ni kwamba inawezekana! Huo ni ujumbe pekee! Nadhani iwapo kila mtu anaweza kujizatiti kufikia amani, na watu kurejea kwenye maisha yao ya kawaida na maendeleo kwa amani, inawezekana. Lakini hilo halipatikani kirahisi na si jambo ambalo jamii ya kimataifa inaweza kufanya pekee au Umoja wa Mataifa, bali wananchi na serikali ni lazima wakubali, na Sierra Leone ilikuwa hivyo! Sekta zote; mashirika yasiyo ya kiserikali, vyama vya kisiasa, viongozi wa kidini, awamu zote za serikali na wadau wote wa kimataifa.”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter