Wakuu wa WFP na UNHCR wawasili Juba

31 Machi 2014

Katika harakati za kubaini hali halisi inayowakumba wananchi wa Sudan Kusini tangu mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yazuke nchini humo tarehe 15 Disemba mwaka jana, hii leo wakurugenzi wakuu wa mashirika ya usaidizi ya Umoja wa Mataifa wamewasili mjini Juba, kwa ziara ya siku mbili.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York ziara hiyo inafanyika wakati zaidi ya watu Laki nane wamepoteza makazi yao tangu kuzuka kwa mapigano ambapo kati yao zaidi ya Elfu Sitini na watano wamejihifadhi kwenye ofisi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini ilhali zaidi ya Laki Mbili wamesaka hifadhi na chakula nchi jirani.

(Sauti ya Dujarric)

“Mkurugenzi mtendaji wa WFP Etharin Cousin na Kamishna Mkuu wa UNHCR Antonnio Gutteres watakuwepo Sudan Kusini kwa siku Mbili kukutana na wakimbizi, wadau na mamlaka husika kabla ya kuvuka mpaka ili kukutana na zaidi ya wakimbizi Elfu Themanini walioko Ethiopia.”

UNHCR na wadau wake imetoa ombi la zaidi ya dola Milioni 370 kusaidia wakimbizi wa Sudan Kusini walioko Kenya, Ethiopia, Sudan na Uganda.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter